Mwanzo Historia Ya Katiba Machapisho Ya Katiba Soma & Pakua Katiba FAQs

                  

UTANGULIZI

 

KWA KUWA, sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayoheshimu na kuzingatia misingi ya utu na udugu, uhuru, kujitegemea, haki, usawa, amani na utulivu, umoja na mshikamano katika nyanja zote za maisha yetu;

 

NA KWA KUWA, tunaamini kuwa misingi hiyo inaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye mfumo wa demokrasia na misingi ya utawala bora ambayo Serikali yake inasimamiwa na Bunge lenye Wabunge waliochaguliwa na wanaowakilisha wananchi, na Mahakama huru inayozingatia misingi ya utoaji haki na kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa na kudumishwa na kwamba uhuru na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu;

 

NA KWA KUWA, tunatambua umuhimu wa kutunza mali za Mamlaka ya Nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuhimiza matumizi bora na endelevu ya rasilimali na maliasili zetu pamoja na kulinda na kuhifadhi mazingira yetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo;

 

NA KWA KUWA, tunatambua umuhimu na faida za kujenga, kukuza na kuendeleza amani, umoja, ujirani mwema na ushirikiano na mataifa mbalimbali ya Afrika na dunia kwa ujumla;

 

NA KWA KUWA, azma ya kujenga Umoja wa Bara la Afrika inadhihirishwa na Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar;

 

NA KWA KUZINGATIA, urithi tulioachiwa na Waasisi wa Taifa letu wa kujenga nchi yenye umoja wa watu wake ambao hawabaguani kwa misingi ya ukabila, dini, rangi, jinsi, ulemavu au ubaguzi wa aina nyingine yoyote;

 

NA KWA KUWA, ni muhimu kulinda, kuimarisha na kuudumisha Muungano, kujenga Taifa huru na linalojitegemea, kuimarisha na kuendeleza misingi ya utawala bora na maadili ya viongozi, kujenga umoja na mshikamano utakaowezesha kutimiza malengo ya Taifa, kujenga na kuendeleza ukuu wa mamlaka ya wananchi, utii wa mamlaka ya Katiba na kuimarisha na kudumisha uzalendo kwa Taifa miongoni mwa Watanzania;

 

NA KWA KUZINGATIA, uzoefu wa zaidi ya Miaka Hamsini ya Muungano, na umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika utungaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

HIVYO BASI, KATIBA HII YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ILIYOPENDEKEZWA NA BUNGE MAALUM LA KATIBA, imetungwa na SISI WANANCHI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA kupitia KURA YA MAONI kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo, na kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia, utawala wa sheria, kujitegemea na isiyofungamana na dini.